Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), aliwapandisha kizimbani vigogo wanne wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba (IMTU) na baadaye kuwaondolea mashitaka kupitia hati ya Nole ya kuwaondolea mashtaka ya kushindwa kufukia viungo vya binadamu na kupeleka hati ya kufukia viungo vilivyotumika kufundishia kwa Kampuni Coroner. 
 Vigogo hao ni, Venkat Subbaian (57), Appm Shankar (64), Prabhakar Rao (59) na Dinesh Kumar (27) ambao walisomewa mashtaka yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, jijini Dar es Salaam leo  saa 8:07  mchana.  Washtakiwa hao walisimama kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kwey Lusemwa. 
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Magoma Magina alidai kuwa Julai 20, mwaka huu washtakiwa wakiwa na nyadhifa  tofauti, Profesa, Mtawala na wahadhiri, kwa makusudi walishindwa kufukia mifuko 83 iliyokuwa na viungo vya binadamu kinyume cha sheria ya 128 kifungu cha 8 na cha 9 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). 
 Magina alidai kuwa katika shitaka la pili, washtakiwa wote kwa pamoja walishindwa kupeleka hati ya kumtarifu kwamba wamefukia viungo hivyo baada ya kutumika kufundishia kama sheria inavyowataka. Hakimu Lusemwa alisema washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili raia wa Tanzania kila mmoja. 
Hata hivyo, kabla mahakama haijasikiliza kipengele cha dhamana, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Salum Ahmed aliwasilisha hati ya Nole kutoka kwa DPP akidai kuwa anawaondolea vigogo hao mashtaka na kwamba hana nia ya kuendelea kuwashitaki. 
 Ahmed alidai kuwa DPP anawaondolea washtakiwa mashitaka hayo chini ya kifungu cha 91 kidogo cha (1) cha CPA kwa kuwa hana nia ya kuendelea kuwashitaka. 
 Wakili wa washtakiwa Gaudiosus Ishengoma alisema kwamba inaonekana kuna mbinu kubwa dhidi ya washtakiwa. Alisema anavyofahamu kwamba hati ya mashitaka ingekuwa na kasoro wateja wake wangepata dhamana na baadaye ingewezekana kubadilishwa. 
Alisema kutokana na sababu hiyo, ana wasiwasi kwamba inawezekana DPP ana nia ya kuwafungulia wateja wangu kesi yenye mashitaka yasiyokuwa na dhamana ili wakasote mahabusu. 
 Viwanja vya mahakama hiyo vilikuwa tulivu huku wanaodaiwa kuwa wafanyakazi wa IMTU wakiwa wamesimama katika makundi makundi wakijadiliana hili na lile. 
Kupitia magari ya Jeshi la Polisi, T 366 AVG aina ya Rav4 alipanda mshtakiwa wa tatu kwa madai kuwa ni mgonjwa na washtakiwa wengine waliondoka mahakamani hapo katika gari yenye namba za usajili KX06EFY aina ya Toyota Landcruiser na kurudishwa mahabusu ya jeshi hilo.
 Washtakiwa wakiwa katika gari la polisi 
 Wakipanda gari baada ya kusomewa mashitaka
 Wakitoka mahakamani baada ya kusomewa mashitaka
 
Washtakiwa wakisubiri kuingia mahakamani.
Picha na Sultani Kipingo wa Globu ya Jamii

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 28, 2014

    Sasa waliwapeleka mahakamani kwa sababu gani? Ina maana DPP alikuwa hajui mwenendo wa kesi? Ni lini serikali itashinda kesi? Nchi nyingi kabla ya kupelekwa mahakamani wanajua kabisa kama kuna kesi ya kujibu au hakuna...sasa kama walikuwa hawana walipelekwa mahakamani kufanya nini? Nionavyo mimi angalau kwenye kesi hii wangetozwa faini hata ndogo kwa sababu tayari hilo ni kosa kutupa cadaver kwenye dampo na haijalishi mfanyakazi yupi alitelekeza hizo cadaver kwenye dampo lakini taasisi ina makosa kama taasisi na ingepaswa kutozwa faini ya usumbufu. Nina wasiwasi na uwezo wa DPP kama kweli anafanya kazi yake kwa weledi inaonekana anafanya kazi kama ni taasisi yake mwenyewe au amehongwa.INASIKITISHA.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 28, 2014

    mdau hapo juu acha kukurupuka soma habari hiyo uielewe vzr, imeandikwa kwa kiswahili fasaha tu sio kwa lugha ya kigeni. kukusaidia tu washtakiwa bado wako rumande watapelekwa mahakamani kwa hati mpya ya mashtaka.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 29, 2014

    Mdau wa pili ndiyo huelewi anachokihoji mdau hapo juu...kama ni kiswahili basi wewe ndiyo usieelewa..mdau anahoji uwezo wa DPP. .kama kweli ni mueelewa mzuri wa kazi yake ni kwa nini amewafikisha mahakamani ilhali akielewa mashitaka yake yana Kasoro? Serikali inaingia gharama nyingi kuwashtaki wahalifu kwa hiyo ni vyema DPP akajipima kabla ya kukurupuka:( ni wazi amekurupuka hapa ndiyo maana amefuta mashitaka..kwa maana nyepesi anajisahihisha ikiwa amechelewa:( mahakamani si mahala pa kuchezea namna hii..washtakiwa wana haki pia..ni mazoea na kawaida yetu kuchelewesha haki za watu kwa makosa ya kisheria yanayoepukika:( DPP lazima awe mtu makini siyo kukurupuka :(

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...