Tuzo za bodi yenye uongozi bora katika sekta ya kibenki na bima zijulikanazo kama Best Board Leadership Awards (BBLA) zinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kesho, ambapo taasisi saba zitashiriki katika tuzo hizo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam hapo jana, Mratibu wa tuzo hizo, Bi. Neema Gerald, amezitaja benki zilizothibitisha kushiriki katika tuzo hizo kuwa ni pamoja na Benki ya Posta (TPB), Benki ya Exim na Benki ya CRDB.
“Kwa upande wa makampuni ya bima, watakaoshiriki ni Heritage Insurance, Alliance Insurance Corporation, Alliance Life Assurance na Strategis Insurance (T) Limited,” alisema.
Kwa mujibu wa Bi. Neema, tuzo hizo maalum kwa ajili ya sekta za kibenki na bima ni mpango pekee uliopo unaolenga kutambua mchango wa uongozi bora wa Bodi za Wakurugenzi katika sekta hizo mbili.
“Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa makampuni yaliyoonyesha mwamko wa kushiriki. Tuzo hizi zinalenga kutambua mchango mkubwa unaotolewa na kundi la watu waliokabidhiwa dhamana ya kufanya maamuzi kwa niaba ya wanahisa,” alisema.
Kwa mujibu wa mratibu huyo, Tuzo hizi zitatoa fursa ya ufahamu ni kwa jinsi gani bodi bora inaweza kusaidia taasisi kupata mafanikio na kufikia utendaji bora hususani katika eneo walilobobea kiutalaam.
"Tumeona umuhimu wa kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na wakurugenzi wa bodi katika taasisi zao. Tunaamini kuwa katika kila mafanikio ya taasisi ya kifedha, nyuma yake kuna bodi ya wakurugenzi imara na makini. Sasa, sifa hizi ambazo wajumbe wa bodi wengi wanakua nazo zinapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa, " alisema.
Akizungumzia tuzo hizo, Bw. Laurence Mwangoka, Meneja Mauzo wa Hoteli ya Serena, ambayo ni moja kati ya wadhamini, alisema kuwa tuzo hizo zimeanzishwa wakati muafaka nchini kipindi ambapo sekta za Bima na kibenki zinapitia mabadiliko makubwa katika ukuaji wake.
Mbali na Hoteli ya Serena, wadhamini wengine wa tukio hilo la kipekee ni pamoja na Excel Management and Outsourcing, Fix Agency Ltd, IPP Media,Real PR Solutions, Lilacnshades, Afrimax Strategic Partnerships Limited na Capital Plus International huku wadhamini zaidi wakiaswa kujitokeza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...