Na  Bashir  Yakub.

Kifungu  cha  112 ( 1 )  na  ( 2 ) cha Sheria  ya Mwenendo  wa  Kesi  za  Jinai   kinaeleza  kwa  urefu  kuhusu  hati  ya  kumkamata  raia ( warrant  of arrest ) ambayo  hutolewa  na  mahakama. Kifungu  hiki  kimeeleza  namna  hati  hii  inavyopaswa kuwa  na  maudhui  yanayopaswa kuwa  ndani ya  hati  hiyo.   

Lengo  ni  kumfanya raia  ajue anakamatwa  na  nani , kwanini  na anapelekwa  wapi. Ni  hati ambayo  imebeba  taarifa  zinazolenga kusimamia  na   kulinda  haki  za  mtuhumiwa . Yumkini  mengi   yaliyo  katika  hati  hii  huwa  hayatekelezwi  na  wahusika.  Raia  wajue  kuwa amri  ya  kukamatwa  kwa mtu  inapotolewa  na  mahakama ni  lazima  askari  anayekuja  kukamata  awe  na  hati  hii.  

 Asije  askari  kukukamata  kwa maelezo  kuwa  ametumwa  na  mahakama  wakati akiwa  hana  hati  hii. Nisisitize tena kuwa  amri  ya  kumkamata  raia inapotolewa  na  mahakama mkamataji  askari  lazima  aje  na hati  hii  kwa ajili  ya  kutekeleza  kazi  hiyo.   Na  ili  hati  iwe  halali  lazima  iwe  na  taarifa  zifuatazo  kama  tutakavyoona  hapa  chini.

1.      HATI  LAZIMA  IWE  NA  TARIFA  HIZI.

( A ) LAZIMA   HATI  YA  KUKAMATA   IANDIKWE  NA  JAJI  AU  HAKIMU.
Upo  utaratibu  ambao  umezoeleka  ambapo  makarani  wa  mahakama  huandika hizi hati.  Hili  ni  kosa  kubwa  kwani  kifungu  hichohicho  cha  112  cha Sheria ya  Mwenendo  wa  Kesi  za  Jinai  kimeweka  wazi  kuwa  hati  ya kukamata  ni  lazima  iandaliwe  na  hakimu  au  jaji. 

 Afisa  yeyote  wa  mahakama  ambaye si  hakimu  au  jaji    hana  kabisa  mamlaka  ya kuandaa  hati  hiyo.  Basi  kama  ndio  hivyo  ieleweke  kuwa  hati  yoyote ambayo  haikuandaliwa  na  hakimu  au  jaji  ndio hati  batili na  ukamataji  unaotokana  na  hati  hiyo   ni  ukamataji  haramu. 

Nimeeleza  katika  makala  zilizopita  kuwa  sheria  inamruhusu  raia  kugomea  ukamataji  ambao  ni  haramu  kama  huo.  Hivyo  niseme tena  kuwa  ikiwa  hati  ya  kukamata  haikuandaliwa  na hakimu au  jaji  basi   raia  anayo  haki  ya  kugomea  kukamatwa.

(  B )  LAZIMA  HATI  YA  KUKAMATA  IWE  NA  MUHURI  WA  JAJI  AU  HAKIMU . 

Kawaida   kila  mahakama  ina  muhuri  wake  ambao  huwa  na  utambulisho  wa  Mahakama  husika.  Muhuri  huo  huwa  nao  jaji au  hakimu wa  mahakama  husika.  Muhuri  huo  ndio  unaotakiwa  kuwa  katika   hati  ya  kukamata. Kama   ni  hati  imetolewa  na  mahakama  kuu  muhuri  uoneshe  kuwa  ni wa mahakama  kuu  halikadhalika  mahakama  nyinginezo  kama za  wilaya  na  mwanzo.

(  C  ) HATI  YA  KUKAMATA  LAZIMA  IONESHE  KOSA  LA  MTUHUMIWA  KWA  UFUPI.

Mpaka  hati  inatolewa  kunakuwa  na  kosa  ambalo  tayari  raia  ametuhumiwa  nalo.  Hati  hii  haiwezi  kutolewa  iwapo  hakuna  kosa  ambalo   limeanzishwa. Kutokana  na  hilo  ni  lazima  kosa  hilo  lioneshwe ndani ya  hati  hiyo  ili  mtuhumiwa  ajue  anakamatwa  kwa  ajili  ya  nini  ili  naye  ajue anaandaa  nini  na  nini  kuhusu  kosa  hilo. Kwa  mfano kosa  liandikwe hivi, KUUA  KWA  KUKUSUDIA  KINYUME  NA KIFUNGU 196  CHA  KANUNI ZA  ADHABU. 

( D ) LAZIMA  HATI  IONESHE  JINA   LA  MTUHUMIWA  AU  WASIFU  WAKE.
Isiwe  hati  imetolewa kwa  ajili  ya  JOHN  ikatumika  kumkamata  CLEMENT.  Aliyeandikwa  kwenye  hati  ndiye  huyohuyo  anayepaswa  kukamatwa. Hii  ndio  sababu  ya  hati  hiyo  kuwa  na  jina. Kama  haina  jina  basi  iwe  inachambua  wasifu  wa  mlengwa  kwa  namna  hivyo hivyo  alivyo. Kama  haina  jina  au  wasifu    wa  mlengwa  basi  hati hiyo  sio  halali  na  mtuhumiwa anaweza  kuigomea.

( E ) LAZIMA  ITAJE  JINA  LA  ASKARI/AFISA   ALIYETUMWA  KUKAMATA .

Si  kila  askari  anamkamata  anayemtaka. Hati  ya  kukamatwa  hueleza  askari/afisa  maalum  aliyepewa  wajibu  wa  kukamata  mhusika.  Itamtaja  kwa  jina   kuwa  huyu  ndiye  aliyepewa  mamlaka  ya  kumkamata  fulani.

Haya  yote  ni  kwa  mujibu  wa  kifungu cha  112 ( 1 ) ( 2 )   cha  Sheria  ya  Mwenendo  wa Kesi  za  Jinai. ACHA  KUNYANYASWA, CHUKUA  HATUA.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

KUSOMA  ZAIDI  LINKS goes  to  sheriayakub.blogspot.com.
              

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...