Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imeahidi kuipa shule ya Sekondari ya Montofort iliyo Yombo Vituka, Dar es Salaam, Tsh. Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa maabara huku ikiwataka wanafunzi wasomee  pia usafiri wa anga kwani sekta hiyo inahitaji wataalam marubani, wahandisi, watoa huduma kwenye ndege n.k.

Ahadi hiyo ilitolewa na Mwanasheria Mkuu wa TAA, Wakili Ramadhan A. Maleta katika mahafali ya kidato cha nne cha shule hiyo iliyo jirani na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere. Shule hiyo inamilikiwa na Kanisa Katoliki na ni moja ya shule bora kielimu katika mkoa wa Dar es Salaam.

Wakili Maleta aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Suleiman S. Suleiman alisema TAA inatoa fedha hizo ikiwa ni mwendelezo wa jitihada zake katika kushirikiana na majirani zake  kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuwataka wanafunzi kushirikiana na TAA kupiga vita ugaidi.

Alisema hivi sasa dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya ugaidi tukio kubwa likiwa la hivi karibuni nchini Ufaransa ambapo yanatishia usalama wa viwanja vya ndege na abiria wanaosafiri. Hivyo, alisema, wanafunzi hao na wengine, wanao wajibu wa kushirikiana na jamii kutoa taarifa zinazosaidia kudhibiti vitendo vya ugaidi.

“Tumekubali kuja kushirikiana nanyi kwa sababu tunafahamu kuwa, ninyi ni washirika wazuri katika vita dhidi ya ugaidi, madawa ya kulevya na kama majirani, ni walinzi wakubwa na muhimu katika viwanja vyetu vya ndege. Mkiona kitu au matukio yasiyo ya kawaida yanayotishia usalama wa ndege, tujulisheni mapema iwezekanvyo,” Wakili Maleta aliwaambia.

Aidha aliwapongeza wahitimu na kuwataka kujiendeleza zaidi kwani kwa dunia ya leo, elimu ya kidato cha nne ni mwanzo tu wa safari ndefu ya kupata maarifa. “Kidato cha nne kiwe mwanzo wa kwenda kidato cha tano na sita na hatimaye chuo kikuu, “ alisema na kuwataka wazazi wajijengee utaratibu wa kuwarithisha watoto wao elimu badala ya mali pekee.

Mwalimu wa Taaluma, Ndugu  Chiku Sekilasi alisema tangu shule hiyo ianzishwe, imekuwa ikifanya vizuri katika taaluma ambapo mwaka 2013, katika mtihani wa kidato cha nne kitaifa, wanafunzi 11 walipata daraja la kwanza, 23 la pili, 17 la tatu na hakukuwa na daraja la nne wala 0 kati ya wanafunzi wote 51.

Alisema mwaka 2014, kati ya wanafunzi 39 waliofanya mtihani wa kitaifa kwa muundo mpya, 5 walipata daraja la juu (distinction), 13 merit, 17 credit na 2 pass na hakuna aliyefeli na kwamba wanatarajia mwaka huu matokeo yatakuwa bora zaidi kutokana na juhudi za pamoja zilizoonyeshwa na walimu na wanafunzi husika.

Mkuu wa shule hiyo, Bruda Dkt. Jim Madavana aliishukuru TAA kwa kuwasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa maabara na kuomba wasamaria zaidi wawasaidie. Wanafunzi walikabidhiwa vyeti huku wale bora wakipewa zawadi ambapo kinara alikuwa Ndugu Emmy Bosco aliyewazidi wenzake katika masomo yote.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA UHUSIANO TAA
DAR ES SALAAM
 24.11.2015

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...