Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akiwa na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Tonia Kandiero (kushoto) mara baada ya kumaliza kikao kilichofanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, jijini Dar es Salaam. Kikao kilijadili masuala mbalimbali ya uendelezaji wa Sekta ya Nishati nchini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akiwa na watendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) waliofika katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, jijini Dar es Salaam ili kujadili masuala mbalimbali ya uendelezaji wa Sekta ya Nishati nchini. Wa kwanza  kushoto ni Afisa Mwandamizi anayeshughulikia Nishati, Stella Mandago na katikati ni Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Tonia Kandiero.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiongoza kikao kati ya watendaji wa Wizara, Taasisi zilizo chini ya Wizara na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, jijini Dar es Salaam. Kikao kilijadili masuala mbalimbali ya uendelezaji wa Sekta ya Nishati nchini. Kulia kwa Waziri ni Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Tonia Kandiero.

Na Teresia Mhagama

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeipongeza Tanzania baada ya nchi ya Uganda kuamua hivi karibuni kuwa Bomba la Mafuta Ghafi lenye kipenyo cha inchi 24 kutoka Hoima nchini Uganda litapita katika ardhi ya Tanzania hadi  bandari ya Tanga.

 Pongezi hizo zilizotolewa na Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo, Tonia Kandiero wakati alipofika katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam  na kuzungumza na uongozi wa Wizara ukiongozwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo pamoja na watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara.

“Tunawapongeza sana kwa kupata mradi huu muhimu kwa nchi ya Tanzania, napenda kukutaarifu kuwa Benki  ya Maendeleo ya Afrika ipo tayari kufanya kazi nanyi ili mradi huo uweze kutekelezeka kama ilivyopangwa,” alisema Kandiero.

Akizungumzia utekelezaji wa bomba hilo la mafuta litakalokuwa na urefu wa kilometa 1403, Profesa Sospeter Muhongo  alisema kuwa, hatua inayofanyika sasa ni majadiliano ya wataalam kutoka nchi hizo mbili juu ya mpango wa utekelezaji wa mradi huo ikiwemo masuala ya fedha na watatoa taarifa yao kwa viongozi wa juu wa nchi hizo.

Alisema kuwa pia kitajengwa kiwanda kwa ajili ya kusafisha mafuta ghafi katika eneo la Hoima nchini Uganda ambapo mradi huo utagharimu Dola za Marekani bilioni 4.7  na kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki atakuwa na hisa ya asilimia 8 na kuwajibika kuchangia Dola za Marekani milioni 150.4  ili kutekeleza mradi huo.

“ Sisi kama nchi tunajipanga kuchukua asilimia zote Nane (8) za hisa hizo na  fedha ambazo tunapaswa kutoa kwenye mradi huu zinaweza kutoka serikalini au Sekta Binafsi hivyo tunaweza kuja AfDB kuzungumza suala hili,” alisema Profesa Muhongo.

Aidha katika kikao hicho, AfDB iliipongeza TANESCO kwa kutekeleza mikakati mbalimbali inayopelekea deni la Shirika kupungua.

 Watendaji wa Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika pamoja Wizara pia walijadiliana  masuala mbalimbali yaliyolenga  kuendeleza miradi ya  Nishati nchini  pamoja na upunguzaji wa deni la TANESCO ili kuliwezesha Shirika hilo kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Aidha Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo, alieleza kuwa AfDB inatoa kipaumbele katika uendelezaji wa miradi ya Nishati ili kuliwezesha Bara  la Afrika kuwa na nishati ya  umeme ya uhakika na kwamba wataendelea kutoa ushirikiano  kwa Wizara ya Nishati na Madini ili kuendeleza miradi ya Nishati pamoja na mafunzo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...