THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

MAKAMU WA RAIS KUONGOZA UPANDAJI MITI KESHO JIJINI DAR


Na Chalila Kibuda, Globu ya jamii

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa upandaji miti Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema upandaji wa miti unaanza kesho hivyo kila mwananchi wa Dar es Salaam anatakiwa kupanda mti mmoja ikiwa ni kwa ajili ya ustawi wa afya.

Amesema kuwa upandaji miti utafanywa katika Wilaya yaTemeke kwa kupanda miti katika barabara ya Kilwa na baada kupanda miti atakagua miundombinu ya maji kwa ajili ya kumwagilia miti katika Wilaya Ilala pamoja na Kinondoni.

Makonda amesema miti hiyo itakayopandwa ni faida ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili hewa na pamoja na vivuli vya kupumzika.Aidha amesema kila mwananchi lazima afanye jitihada za kupanda miti ikiwa ni pamoja watendaji wote wa mitaa na kata kuhamasisha wananchi kupanda miti.

Hata hivyo amewataka mashabiki wa yanga na simba kupanda miti kabla ya kuanza mpira kati timu hizo.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza leo na waandishi habari juu ya upandaji miti utaozinduliwa kesho,jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka Globu ya Jamii)


WAZIRI MKUU APOKEA MICHANGO YA SH. MILIONI 190.

 Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akipokea hundi ya shilingi milioni 80 kutoka kwa Balozi wa Pakistan nchini, Amir Khan  (wapili kushoto ukiwa ni mchango  kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani  Kagera. 
Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye hoteli ya Kyatt Regency jijini Dar es salaam Septemba 30, 2016. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Augustine Mahiga na  kulia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya Shilingi milioni 50 kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Tasisi ya Aga khan nchini, Amin Kurji (kulia) ukiwa ni mchango kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 30, 2016. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Augustine Mahiga na wapili kulia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako. 
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea jumla ya sh. milioni 190 kutoka kwa balozi wa Pakistan nchini Mhe. Amir Khan, Kaimu Balozi wa China Mhe. Gou Haodong na Taasisi ya Aga Khan.

Fedha hizo zimetolewa ili kusaidiia  wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa.

Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

Makabidhiano ya michango hiyo, yamefanyika leo (Ijumaa, Septemba 30, 2016) kwenye Hotel ya Hyatt Regency jijini Dar Es Salaam ambapo Waziri Mkuu aliwashukuru kwa michango hiyo na alitumia fursa hiyo kuwaomba wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi zao.

“Ninawaomba wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi kwa kuzileta ofisini kwangu au kutuma kupitia akaunti ya maafa iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz,” amesema.

Amesema watu walio mbali na benki watumie namba za simu zilizotolewa mahsusi kwa ajili ya kupokea michango ya maafa hayo ambazo ni 0768-196-669 (M-Pesa), au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).

Akikabidhi hundi kwa Waziri Mkuu, Balozi wa Pakistan, Mhe. Amir alisema wanaamini mchango huo wa sh. milioni 80 walioutoa utasaidia kuwapunguzia uchungu wananchi wa Kagera kutokana na athari zilizosababishwa na tetemeko la ardhi.

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa China Mhe. Haodong alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameshtushwa na tukio hilo na tayari walishawapeleka madaktari na wataalamu wengine mkoani Kagera na leo walikuwa wanakamilisha ahadi yao ya kutoa mchango wa sh. milioni 60.
Naye Muwakilishi Mkazi wa Taasisi za Aga Khan nchini, Amin Kurji  alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 50.                               
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
IJUMAA, SEPTEMBA  30, 2016.


TAASISI 10 ZA SERIKALI ZIMEFANYA CHINI YA KIWANGO YA SHERIA YA MANNUZI YA PPRA.

  Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Matern Lumbanga akizungumza na waandishi wa habari juu ya ukaguzi waliofanya katika taasisi za serikali katika kufuata sheria ya manunuzi leo jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Matern Lumbanga jijini Dar es Salaam leo.

Na  Yassir Adamu, Globu ya Jamii.
RIPOTI ya Ukaguzi kwenye manunuzi ya umma ya mwaka wa fedha 2015/2016 uliofanywa na mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) unaonyesha taasisi  10  nunuzi  zimefanya  manunuzi chini ya kiwango kisichoridhisha chini ya asimia 60.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Matern Lumbanga amesema taasisi hizo zimefanya chini ya kiwango katika kufanya manunuzi  yake  kwa  mujibu wa sharia ya manunuzi.

Amesema jumla ya PPRA imefanya  jumla ya mikataba 21,313 ya manunuzi yenye thamani ya sh.Trioni 1.05 katika ujenzi ,vifaa, huduma ushauri wa kitaalam .huduma zilizohitaji mikatba ya ushauri wenye thamani ndogo  pamoja na mikataba yenye makubaliano maalum.

Balozi Lumbanga amezitaja taasisi zilizofanya chini ya kiwango ambazo ni Taasisi ya Uzalishajin (NIP), Dar es Salaam Rapid Transist (DART), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Makumbusho ya Taifa, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Taasisi ya Mifupa (MOI), Halmashauri ya Manispaa ya Msoma pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Bukoba (Buwasa).  

Amesema mikataba 122 ya ukusanyaji wa mapato iliyokaguliwa kwenye mamlaka tisa ya serikali za mitaa kwa mujibu wa mikataba iliyokaguliwa imebainika kuwa na mapungufu kadhaa katika usimamizi wa mikataba hiyo na kufanya halmashauri kushindwa kukusanya kiasi cha sh. Milioni 761.54.

Aidha Balozi Lumbanga amesema kuwa kushindwa kukusanya mapato hayo Halmashauri zimesababisha hasara halmashauri hizo zimeshindwa kuchukua hatua zozote dhidi ya wazabuni waliopewa miradi kutokana mikataba walioingia.


MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZEE DUNIANI KUADHIMISHWA KESHO.

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZEE DUNIANI TAREHE 1/10/2016

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, inatoa taarifa kuwa, tarehe 1 Oktoba ya kila mwaka, ni kilele cha  Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani. Katika siku hii, Tanzania inaungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku hii kwa mujibu wa Azimio la Umoja wa Mataifa Na. 49 la mwaka 1991.  

Maadhimisho ya siku ya wazee duniani ni moja kati ya jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) katika kutambua na  kuhamasisha jamii kuweza kulinda na kutetea haki za wazee duniani kote.  Umoja wa Mataifa umetenga siku hii kwa lengo la kutafakari hali ya maisha ya wazee na changamoto zinazowakabili wazee; na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuboresha maisha yao na kuwafanya waishi maisha ya heshima, hadhi, na kuthaminiwa utu wao.  

Kila mwaka, Maadhimisho haya huwa yanabeba Kauli Mbiu yenye ujumbe mahsusi. Kwa mwaka 2016 Kaulimbiu inasema “Zuia Unyanyasaji dhidi ya Wazee”. Kaulimbiu hii inahimiza Serikali, jamii, na wadau wengine kutafakari na kuweka mikakati ya kukabiliana na vitendo vya ukatili, mauaji, ubaguzi na dhuluma dhidi ya wazee; vitendo ambayo ni kinyume dhidi ya haki za binadamu. 
Maadhimisho haya kwa mwaka 2016 yanafanyika Kitaifa katika wilaya ya Mbalali, mkoani Mbeya. Kilele cha maadhimisho haya kitajumuisha shughuli mbalimbali ikiwemo huduma ya upimaji wa hiari wa afya na ushauri kwa wazee, michezo na maonesho ya bidhaa na kazi mbalimbali zinazofanywa na wazee. 
Katika kipindi hiki cha Maadhimisho hatuna budi kuenzi na kudumisha mila na desturi nzuri za kuwaenzi wazee kwa kutambua kuwa wazee ndiyo chanzo cha urithi wa historia ya nchi, washauri wa familia na jamii, watu wenye hekima, na walezi katika jamii. Hivyo jamii inaowajibu wa kuwaondolea vikwazo wazee katika kupata huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua pale ambapo mzee ananyanyashwa au kutendewa isivyostahili.  

Erasto T. Ching’oro
Msemaji wa Wizara
30/9/2016.


TFS YASAIDIA MADAWATI 12,000 MKOANI MWANZA.

 Naibu  Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii , Eng.  Ramo Makani( kushoto)  akimkabidhi  madawati  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela ( kulia) ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa bungeni mwanzoni mwa mwaka huu na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe ya kutengeneza madawati 20,000,  wa  pili kushoto  ni Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo.
 Baadhi ya madawati yaliyokabidhiwa  jana  na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongela  ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa bungeni mwanzoni mwa mwaka huu na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe ya kutengeneza madawati 20,000.
Baadhi ya wanafunzi wakiwa wamekaa kwenye madawati mara baada ya makabidhiano yaliyofanyika Mkoani Mwanzan jana  na Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani  kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza , John Mongela  ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa bungeni mwanzoni mwa mwaka huu na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe.

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imekabidhi madawati 12,115 mkoani Mwanza ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa bungeni mwanzoni mwa mwaka huu na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe ya kutengeneza madawati 20,000.

Makabidhiano hayo baina ya TFS na Serikali yalifanyika kitaifa kwenye Uwanja wa chuo cha Mafunzo ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi.

Naibu wa Waziri wa Wizara hiyo , Ramo Makani alitoa mwezi mmoja kwa uongozi wa TFS kuhakikisha unakamilisha kutengenenza madawati 7,885 yaliyosalia kabla ya novemba mwezi huu

‘’ Pamoja na kufikia asilimia 61 ya lengo, nawaomba TFS muhakikishe idadi iliyobaki ya madawati inakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao’’ Alisema Makani.
Akizungumza kabla ya kukabidhi madawati hayo, Mtendaji Mkuu wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo bila kutaja gharama iliyotumika alisema ofisi yake imechelewa kufikia asilimia 100 ya kutengeneza madawati 20,000 kutokana na kuwa na changamoto ya ucheleweshwaji wa taratibu za uvunaji mbao katika baadhi  ya misitu.

TFS tumetekeleza agizo hili kwa kulenga ngazi za chini kabisa za mfumo wa utendaji wa Wakala  ambao ni wilaya. Hivyo katika kugawa idadi ya utengenezaji madawati wa kanda ilizingatia idadi ya wilaya kwa kila kanda’’ alisema Prof. Silayo.

Waziri Makani alisema madawati hayo yatagawiwa katika mikoa ya Simiyu., Kagera, Mara,Geita na Mwanza ambayo itapokea madwati 2,580 yaliyokwisha tengenezwa.

Akizungumz kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela aliwapongeza TFS na kuahidi kuyatunza madwati hayo ili yatumike kwa muda mrefu kwa manufaa ya wanafunzi.
                ( Picha na Lusungu Helela- Wizara ya Maliasili na Utalii)


NAIBU KAMISHNA AKUTANA NA WAKUU WA USALAMA BARABARANI NCHINI (ZTO)

 Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi Mohamedi Mpinga wa pili kulia, akimsikiliza  ZTO kanda maalum ya Dar Es Salaam ACP Awadhi J. Haji aliesimama akizungumza katika kikao cha utendaji kazi kilichowahusisha ZTO nchi nzima, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Alphendo Mkoani Geita kabla ya kuendelea na shughuli za uelimishaji juu ya Usalaam Barabarani wiki ambayo kitaifa inaadhimishwa  Mkoani Humo.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi Mohamedi Mpinga wa pili kulia, akimsikiliza  ZTO kanda maalum ya Dar Es Salaam ACP Awadhi J. Haji aliesimama akizungumza katika kikao cha utendaji kazi kilichowahusisha ZTO nchi nzima, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Alphendo Mkoani Geita kabla ya kuendelea na shughuli za uelimishaji juu ya Usalaam Barabarani wiki ambayo kitaifa inaadhimishwa  Mkoani Humo.
(Picha na Trafiki kuu)


KUNDI LA VITIMBI TOKA KENYA LANOGESHA TAMASHA LA 35 LA SANAA BAGAMOYO

 Waigizaji wa Kundi la sanaa la Vitimbi toka nchini Kenya, wakizungumza mara baada ya kutoa moja maigizo yao katika Tamasha la 35 la Sanaa la Utamaduni Bagamoyo, linaloendelea kufanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Sanaa (TaSuBa), Bagamoyo Mkoani Pwani. Wakizungumza na waigizaji hao walisema kuwa wanafuraha sana kushiriki kwenye Tamasha hilo, kwani ni kubwa na la kuvutia sana, pia wametoa wito kwa Waigizaji wa Kitanzania kuungana na wale wa Kenya na kufanya kazi kwa pamoja kwani wanaamini wakiungana wanaweza kufanya kazi nzuri sana.
 Waigizaji wa Sanaa ya Vichekesho kutoka nchini Kenya, Mama Kayaii na Mama wa Mahakama, wakitoa burudani ya moja ya maigizo yao ya jukwaani kwa watazamaji waliojitokeza kwenye Tamasha la 35 la Sanaa la Utamaduni Bagamoyo, linaloendelea kufanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Sanaa (TaSuBa), Bagamoyo Mkoani Pwani.
 Waigizaji wa Kundi la Vitimbi kutoka nchini Kenya, Ondieki, Profesa na Sukuma Wiki wakiigiza jukwaani katika Tamasha la 35 la Sanaa la Utamaduni Bagamoyo, linaloendelea kufanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Sanaa (TaSuBa), Bagamoyo Mkoani Pwani.
Igizo likiendelea.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamadini Bagamoyo (TaSuBa), Dkt. Herbert Makoye (kushoto) akizungumza na baadhi ya Waigizaji wa Kundi la sanaa la Vitimbi toka nchini Kenya, mara baada ya kutoa burudani ya kuvutia kwa WanaBagamoyo, waliofurika kwa wingi kwenye Ukumbi wa Chuo cha Sanaa (TaSuBa), Bagamoyo Mkoani Pwani.


BENKI KUU YA TANZANIA YASEMA PATO LA TAIFA LIMEONGEZEKA KWA ASILIMIA 7.9


Na Dotto Mwaibale

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema ukuaji wa pato la Taifa umeongezeka kwa asilimia 7.9 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.8 kwa kipindi kama hicho mwaka 2015.

Hayo yamebainishwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu Dar es Salaam leo asubuhi wakati akizungumza na wanahabari kuhusu ukuaji wa pato la Taifa kwa robo na nusu mwaka 2016.

Profesa Ndulu alisema shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya juu zaidi katika kipindi hicho ni usafirishaji na uhifadhi wa mizigo ikiwa ni asilimia 30.6, uchimbaji wa madini kwa asilimia 20.5, mawasiliano na habari asilimia 12.6 na sekta ya fedha na bima kwa asilimia 12.5.

Alisema ukuaji wa sekta ya uchukuzi na uhifadhi wa mizigo umetokana na kuongezekea kwa usafirishaji wa abiria kwa njia ya barabara na gesi asilia ambao umekua kwa zaidi ya nusu ukilinganisha na robo ya pili ya mwaka 2015 kwa asilimia 9.4.

"Kwa upande mwingine, ukuaji wa sekta ya uchimbaji wa madini na gesi umechangiwa zaidi na kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi ambao umekua kutoka mmSFt3.7,793 kwa mwaka 2015 mpaka mmSFt3 11,267 kwa mwaka 2016" alisema Ndulu

Profesa Ndulu alitaja sekta nyingine ambayo imefanya vizuri ililinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2015 kuwa ni sekta ya kilimo ambayo imekua kwa asilimia 3.2 kwa robo ya pili ya mwaka 2016 wakati mwaka jana ilishuka kwa asilimia 1.9.

Aidha sekta ya fedha na bima imekua kwa asilimia 12.5 kwa robo ya pili ya mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 10.0 kwa robo ya pili ya mwaka 2015.

Akizungumzia ukuaji wa pato la Taifa alisema katika nusu ya mwaka 2016 yaani Januari hadi Juni 2o16 kasi ya ukuaji wa pato la taifa imeongezeka na kufikia asilimia 6.7 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2015.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandshi wa habari Dar es Salaam leo, wakati akitoa taarifa ya ukuaji wa pato la taifa kwa robo na nusu ya mwaka 2016. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mabenki, Kenedy Nyoni.
Kaimu Meneja Kitengo cha Mahusiano kwa Umma wa BoT, Victoria Msima, akimkaribisha Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu  (wa pili kushoto), kuzungumza na wanahabari kuhusu ukuaji wa pato la taifa kwa robo na nusu mwaka 2015 Dar es Salaam leo.
Taswira ya meza kuu katika mkutano huo. Kutoka kulia ni Kaimu Meneja Kitengo cha Mahusiano kwa Umma, Victoria Msima,Mkurugenzi wa Idara ya  Usimamizi wa Mabenki, Kenedy Nyoni, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Beno Ndulu na Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti wa Sera za Kiuchumi, David Kwimbere.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.


Waziri Nape awatoa wasiwasi mashabiki wa soka kuhusu tiketi za kieletroniki.

Na Raymond Mushumbusi WHUSM.

Mashabiki wa soka nchini wameondolewa wasiwasi kuhusu upatikanaji wa tiketi kuelekea mchezo wa ligi Kuu Tanzania Bara kati ya watani wa Jadi Yanga na Simba na kuhakikishiwa kuwa mfumo wa upatikanaji tiketi uko vizuri na mpaka sasa tiketi zinaendelea kuuzwa katika maeneo mbalimbali.

Wasiwasi huo umetolewa na Waziri wa Habari Utamaduni sanaa na Michezo  Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusu matumizi ya tiketi za kieletroniki kuelekea mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na Simba.

Waziri Nape amesema kuwa kuna kuna taarifa kutoka mitaani kuwa kuna uwezekano wa mfumo huu kutofanya kazi katika mechi hii na malalamiko ya watu wengi kulalamika kukosa tiketi za mchezo wa kesho.

“kwa kila anayetaka kwenda uwanjani kesho kadi zinapatikana nimewaagiza Selcom wahakikishe wanazungusha magari yao mtaani kuangalia mahali penye upungufu na yawe na watu wenye kadi hizo aidha, watu waongezwe kwenye vituo ambayo vina idadi kubwa ya wateja wanaohitaji kadi” Alisema Mhe Nnauye.

Aidha Waziri Nape Nnauye amewahakikishia watanzania kuwa atausimamia mfumo huu kikamilifu na kwa gharama yoyote na atahakikisha   hautakuwa na mapungufu na endapo yatajotokeza yatashughulikiwa na wataalamu ili kuufanya mfumo huu kufanya kazi ipasavyo kama ulivyokusudiwa.

Kwa upande wake Meneja Mradi kutoka Selcom Tanzania Galius Runyeta amefafanua kuwa mfumo huu uko wazi kabisa kwa wadau wote wanaohusika na mapato ya uwanjani na utakuwa njia mbadala ya kudhibiti mapato yatokanayo na mechi.

“ Kwa mfumo huu hakuna njia ya mkato kila kitu kiko wazi na kwa kila dakika utaona mabadiliko ya idadi ya tiketi zinazonunuliwa na mpaka sasa zaidi ya tiketi 10,000 zimenunuliwa na zinazidi kununuliwa” Alisema Runyeta.

Kwa miaka mingi kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau wa soka nchini kuwepo kwa upotevu wa mapato katika mechi za ligi na kimataifa katika viwanja vya soka nchini kwa kuliona hilo Serikali iliamua kuanzisha mfumo utakaomaliza tatizo hilo na kukomesha mianya yote ya ulaji iliyokuwepo katika mfumo uliopita. 
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu maendeleo ya upatikanaji  wa tiketi za kieletroniki  kuelekea mechi ya Ligi kuu Tanzania Bara ya watani wa Jadi  Yanga na Simba itakayochezwa kesho Oktoba Mosi leo ,2016 kushoto ni Meneja Mradi kutoka kampuni ya Selcom Tanzania Bw. Gallius Runyeta.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani)  leo Jijini Dar es Salaam kuhusu maendeleo ya matumizi ya tiketi za kieletroniki  kuelekea mechi ya Ligi kuu Tanzania Bara ya watani wa Jadi Yanga na Simba itakayochezwa kesho Oktoba Mosi leo ,2016. 
 Waziri wa Habari Utamaduni sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akieleza waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu maendeleo ya matumizi ya tiketi za kieletroniki  kuelekea mechi ya Ligi kuu Tanzania Bara ya watani wa Jadi Yanga na Simba itakayochezwa kesho Oktoba Mosi leo ,2016 kulia ni Kaimu kurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo wa Wizara hiyo Bw. Alex Nkenyenge. 
 Meneja Mradi kutoka kampuni ya Selcom Tanzania Bw. Gallius Runyeta akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es  Salaam jinsi ya kutumia  mfumo kununua tiketi za kieletroniki  kuelekea mechi ya Ligi kuu Tanzania Bara ya watani wa Jadi Yanga na Simba itakayochezwa kesho Oktoba Mosi leo ,2016. 


WAZIRI NAPE AKUTANA NA BALOZI WA SPAIN NCHINI.

 Waziri wa Habari, Utamaduni,  Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akizungumza na Balozi wa Spain nchini Bw. Felix Costales Artieda kuhusu kusaidia kuendeleza sekta ya Utamaduni na Michezo leo Septemba 30,2016 wakati Balozi huyo alipofika ofisini kwa Waziri  Jijini Dar es Salaam kukabidhi moja ya mradi wa Utamaduni uliokuwa ukifanywa na serikali ya Spain katika Bonde la Ufa la Olduvai Gorge Mkoani Manyara.
Balozi wa Spain nchini Bw. Felix Costales Artieda (kushoto) akizungumza na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye kuhusu kuendeleza mradi wa kujenga Shule ya Mpira wa Miguu Kigamboni kama ilivyokuwa katika mkakati wa awali alipofika Ofisini kwa waziri Jijini Dar es Salaam  Septemba 30, 2016 kumkaribisha kuwa mgeni rasmi katika maonyesho ya Utamaduni yaliyoandaliwa na nchi ya Spain yatakayofanyika Makumbusho ya Taifa.
Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (kulia) akisoma mradi wa Utamaduni uliokuwa ukifanyika Olduvai Goerge mkoani Manyara baada ya kukabidhiwa na Balozi wa Spain nchini Bw. Felix Costales Artieda (kushoto) Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam Septemba 30, 2016.


TAOMAC wamkabidhi Waziri Mkuu Majaliwa Jumla ya Shilingi 404.8 Milioni kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la Kagera

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wane kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wanachama wa Chama cha Waagizaji Wakubwa wa Mafuta (TAOMAC) baada ya kupokea hundi ya fedha kiasi cha sh. Milioni mia nne na nne na laki nane (404,800,000) pamoja na mifuko ya simenti 1000 kutoka chama hicho kwa ikiwa ni mchango wa wanachama wa chama hicho kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni mkoani Kagera. Wengine ni pamoja na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ,Charles Mwijage (wa kwanza kulia).

========  ======= ========


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea fedha kiasi cha sh. Milioni mia nne na nne na laki nane (404,800,000) pamoja na mifuko 1000 ya simenti kutoka kwa Chama cha Waagizaji Wakubwa wa Mafuta TAOMAC ikiwa ni mchango wa wanachama wa chama hicho kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni mkoani Kagera.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo Waziri Mkuu Majaliwa pamoja na kuwashukuru watu binafsi, taasisi na mashirika yaliyojitoa kwa hali na mali katika kuwasaidia waathirika wa janga hilo, pia aliwahakikishia kuwa misaada wanayoitoa itawafikia walengwa huku akibainisha kuwa serikali imejipanga kuzuia kila aina ya wizi au ubadhilifu wa misaada hiyo.

“Tayari tumechukua hatua kwa wahusika wote waliojaribu kucheza na misaaada hii. Niwahakikishie tu kwamba serikali ipo makini kwenye misaada na michango inayoendelea kutolewa kwa kuwa ni jukumu lake kufanya hivyo kwa kuwa mnapotoa misaada hii maana yake kuna sehemu mmejinyima,’’ alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TAOMAC Bw Salum Bisarara alisema mchango huo ni mwitikio wa ahadi walioyoitoa kwenye mkutano ulioitishwa na Waziri Mkuu Majaliwa na kufanyika Ikulu Septemba 13 nakuhusisha wadau mbalimbali nchini kwa kusudio la kuchangia waathirika wa tetemeko hilo.

“Katika kikao kile Wanachama wa TAOMAC tuliahidi mambo mawili, kwanza wanachama wenzetu watatu ambao ni GBP, OILCOM na MOIL waliahidi kuchangia kwa kuchukua jukumu la kuzijenga upya shule mbili za sekondari zilizoathirika ambazo ni shule ya IHUNGO na ya NYAKATO. Gharama za ujenzi huo tutajulishwa baada ya kukamilika tathmini,’’

“Pili wanachama waliosalia tuliahidi kukutana na kuchangisha fedha ili zisaidie waathirika wa tetemeko kwa njia mbalimbali ikiwemo kutengeneza upya miundo mbinu iliyoharibika hasa zahanati, hospitali, barabara na madaraja, ahadi ambayo tunaikamilisha leo,’’ alisema.

Katika mchango huo jumla ya Sh. Milioni mia mbili na arobaini na nne (244,000,000) tayari zilikuwa zimeingizwa kwenye akaunti maalumu ya kuchangia waathirika hao huku kiasi cha sh milioni mia moja na sitini ((160,000,000) kikiwa ni hundi halisi za kampuni wananchama ambazo zilikabidhiwa kwa mhasibu ofisi ya Waziri Mkuu.

Aliyataja makampuni yalichongia kuwa ni pamoja na Mogas Tanzania Ltd, National Oil (T) LTD, Barrel Petrol Energy, ATN Petroleum Company LTD, Petroafrica (T) Ltd, TSN Oil, Delta Petroleum, Engen Petroleum, Agusta Energy, Petrofuel, Genera Petroleum, Sahara, TIPER, Hass Petroleum, Lake Oil, Dalbit Petroleum, Camel Oil, Gapco, Oryx Oil Company na Puma Energy.

Aidha, wanachama wa chama hicho walimuahidi Waziri Mkuu kuwa wataendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika ujenzi wa taifa letu huku wakiishukuru serikali kwa kuwashirikisha katika kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo.


RAIS WA SHIRIKA LA ENGENDER HEALTH LA MAREKANI AKUTANA NA WAZIRI WA AFYA WA ZANZIBAR.


Rais wa Shirika la Engender Health la Marekani Ulla Muller ambae pia ni Mtendaji Mkuu (CEO) wa Shirika hilo akizungumza na Waziri wa Afya  Mahmoud Thabit Kombo alipomtembelea Ofisini kwake Mnazimmoja Mjini Zanzibar, (kulia) ni Mkurugenzi Ufundi ambae ni Naibu mwakilishi wa Shirika hilo Tanzania Feddy Mwanga.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akiagana na mgeni wake Rais na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Engender Health Ulla Muller baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Waziri Mnazimmoja Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.


SMMRP YAENDELEA KUBORESHA MAJENGO OFISI ZA MADINI


Zuena Msuya, Mtwara

Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ulio chini ya Wizara ya Nishati na Madini, umekabidhi Jengo la kisasa kwa Kanda ya Madini Kusini ambalo linatarajiwa kurahasisha utendaji kazi kwa kutumia mfumo wa teknolojia ya kisasa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi jengo hilo mkoani Mtwara hivi karibuni, Msanifu Majengo wa SMMRP, Joseph Ringo alisema kuwa, ujenzi wa jengo hilo umefadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia mradi huo kwa lengo la kuboresha Sekta ya Madini nchini.

Ringo alisema kuwa, jengo hilo ambalo litatumika kama kituo cha Kisasa cha Madini (Center for Excellence) limeunganishwa katika mfumo wa kisasa wa TEHAMA kwa kuhifadhi taarifa pamoja na kumbukumbu mbalimbali za kidijitali za madini za Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake na endapo itatokea tatizo katika mfumo huo itakuwa ni rahisi kupatikana.

Alifafanua kuwa, jengo hilo limeunganishwa na mfumo wa kisasa wa TEHAMA, Ofisi za watendaji wa wizara, maktaba ya kisasa ya kuhifadhia taarifa za madini yanayopatikana katika ukanda wa kusini pamoja na uwepo wa vyumba maalumu vyenye vifaa kwa ajili ya kutolea mafunzo kwa wachimbaji wa madini.

Aidha, Ringo alifafanua kuwa, mradi wa SMMRP umelenga katika kuboresha miundombinu hasa ya majengo kwa kuweka mifumo ya kisasa pamoja na kuimarisha shughuli za rasilimali madini katika Ofisi za Kanda na Mikoa nchini.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka alisema kuwa hivi sasa jengo hilo litawasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi kwakuwa lina uwezo wa kukidhi miundombinu yote ya wafanyakazi. Vilevile, amewataka wafanyakazi watakaokuwa wakitumia jengo hilo kuitunza na kulinda miundombinu ya jengo hilo.

Jengo hilo limebuniwa na Kampuni ya OGM Architects Consultants na kujengwa na kampuni ya ukandarasi ya Malcom Investment Co Ltd.

Mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Malcom Investment Co Ltd (mwenye tshirt ya bluu) waliojenga jengo hilo, akikabidhi ufunguo kwa Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali watu wa Wizara ya Nishati na Madini Bibi Joyceline Lugora (katikati) wakati wa kukabidhi jengo hilo kwa kanda ya madini kusini mkoani Mtwara hivi karibuni.
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (aliyeshika ufunguo) baada ya kupokea kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali watu wa Wizara ya Nishati na Madini, Joyceline Lugora (katikati) tayari kuanza kulitumia jengo hilo kabla ya kuzinduliwa rasmi hivi karibuni.
Taswira ya muonekano wa upande wa kulia wa jengo hilo la Ofisi ya Madini Kanda ya Kusini mkoani Mtwara. 
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka,(kulia) na Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali watu wa Wizara ya Nishati na Madini Joyceline Lugora wakitia sahihi nyaraka za kukabidhiwa jengo la Ofisi ya Madini Kanda ya Kusini mkoani Mtwara wakishuhudiwa na  Msanifu Majengo wa SMMRP, Joseph Ringo (katikati) 


Wateja wa viwanja vya Bayport Kilwa waanza kupewa hati

Afisa Sheria wa Bayport Financial Services, Mrisho Mohamed katikati akimkabidhi hati yake ya kiwanja mteja wao aliyenunua kiwanja cha Kilwa, Mubarack Kirumirah kulia. Kushoto ni Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

WATEJA wa viwanja vya Bayport Financial Services wilayani Kilwa, mkoani Pwani wameanza kupewa hati zao kutoka mradi wa Kilwa Msakasa unaoendeshwa na taasisi hiyo inayojihusisha na mikopo, huku ikiwa na dhamira ya kuwakwamua wateja wao na Watanzania kwa ujumla.

Mradi wa Kilwa Msakasa ni miongoni mwa miradi kadhaa inayoendeshwa na taasisi hiyo ikiwamo Bagamoyo, Vikuruti, Kigamboni na Kibaha na kujikita kurahisisha pia utoaji wa hati kwa wateja wao waliokamilisha utaratibu rahisi wa malipo ya viwanja hivyo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Masoko na Mawasiliano, Mercy Mgongolwa, alisema kwamba kuanza kutolewa kwa hati za mradi huo wa Kilwa ni sehemu ya mwendelezo wa kuboresha huduma zao za mikopo ya viwanja inayotolewa sehemu mbalimbali nchini Tanzania.


Mteja wa Bayport Financial Services, Mubarack Kirumirah kulia akitia sahihi kabla ya kukabidhiwa hati yake ya kiwanja cha Kilwa. Anayeshuhudia ni Afisa Sheria wa Bayport Financial Services, Mrisho Mohamed.

Shughuri za maandiko ya kukabidhiana hati zikiendelea katika ofisi za Bayport jana.


Alisema taasisi yao imeendelea kuboresha huduma zao ili kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata uwezo wa kumiliki kiwanja chenye hati kwa ajili ya kuvitumia katika mipangilio ya maisha yao.


“Bayport ni taasisi ambayo imekusudia kuona watu wanamiliki viwanja vyenye hati kwa urahisi, hivyo kila aliyekopa kiwanja au kununua kwa fedha taslimu kupitia kwetu atakabidhiwa hati yake haraka iwezekanavyo kwa sababu tumedhamiria kuwakwamua wateja wetu wote, hivyo wale ambao hawajapata fursa ya kuhudumiwa na ofisi yetu wafanye hivyo ili waone namna gani Bayport ipo kwa ajili yao,” alisema Mercy.

Naye Afisa Sheria wa Bayport Financial Services, Mrisho Mohamed, aliwataka wateja wao kutembelea katika ofisi za taasisi yao zilizoenea nchi nzima ili wapate huduma bora za mikopo ya viwanja inayowahusu watumishi wa umma, wafanyakazi wa kampuni binafsi pamoja na wajasiriamali.

“Tunajivunia kufanya kitu tofauti kwa wateja wetu ndio maana kila anayepata kiwanja kwetu tunahakikisha kwamba hapati usumbufu wowote wa kufuatilia hati sehemu husika badala yake sisi ndio tumechukua jukumu hilo tukiamini kwamba jambo hili litakuwa mkombozi kwa wateja wote,” alisema Mohamed.

Naye mteja wa Bayport aliyekabidhiwa hati yake ya kiwanja cha Kilwa, Mubarack Kirumirah Hamidu, aliwashukuru Bayport kwa kufanya kazi nzuri inayowaendelea usumbufu wateja wao kufuatilia hati za viwanja, jambo linaloonyesha utofauti mkubwa katika suala zima la ardhi.

“Nashukuru kwa kupata hati ya kiwanja change kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu tangu nilipojitokeza kununua kiwanja cha Kilwa Msakasa, hivyo suala hili limenifurahisha na kuwaeleza Watanzania wenzangu kuchangamkia kununua viwanja vya Bayport,” alisema.

Wengine waliokabidhiwa hati zao za viwanja vya Kilwa ni Mrina Harish Mawji, Jigar Patel, Amina Haidari Amani, Victoria Ambrose Kundi na wengine wengi ambao wamekuwa miongoni mwa Watanzania waliojitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa ya mikopo ya viwanja vya Bayport vinavyoendelea kutolewa na taasisi hiyo nchini Tanzania.


SERIKALI YAANZA KUFANYA MABORESHO YA KUANDAA NA KUHAKIKI SERA YA UBORESHAJI WA VIWANDA VYA DAWA VILIVYOPO NCHINI

Na Nteghenjwa Hosseah, ARUSHA 

SERIKALI imesema kuwa inaanza kufanya maboresho kwa kuandaa na kuhakikisha Sera ya Uboreshaji wa Viwanda vya Dawa vilivyopo nchini kwa kuwawezesha na kuwajengea uwezo wenye viwanda nchini ili waweze kuzalisha dawa na kupunguza uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo kwa niaba ya Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza katika Kongamano la 49 la Chama Cha Wafamasia Tanzania (PST),linalofanyika jijini hapa kwa siku mbili.

Akizungumza kwa niaba ya Mhagama, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo,alisema kuwa kutokana na umuhimu wa sekta hiyo ya dawa, Serikali inaangalia taaluma hiyo kwa macho mawili kwa lengo la kuiboresha ili iweze kutoa huduma bora.

"Wizara yangu inaangalia taaluma hii kwa macho mawili katika kuhakikisha kuwa sekta ya dawa inaboreka na inakua na hatimaye kuweza kukuza uchumi wetu, kwa kuwawezesha na kuwajengea uwezo wenye viwanda nchini ili waweze kuzalisha zaidi ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia soko ndani ya nchi na kupunguza uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi na hivyo kuwa na dawa bora, salama na zenye ufanisi"

"Endapo tutazalisha dawa zetu wenyewe hii itatupunguzia gharama zisizo za lazima kuagiza dawa nje ya nchi, sambamba na hili pia tunaboresha vyuo vya Wafamasia ili waweze kutoka wataalamu bora wa masuala haya ya madawa,”alisema Gambo

Akizungumzia suala la wizi wa dawa katika hospitali za serikali,alisema kuwa Serikali haina mchezo na yoyote atakayokiuka maadili ya taaluma hiyo na kuwa watawachukulia hatua kali za kisheria ili wananchi wapate huduma bora za dawa. "Mbali na changamoto ya upungufu wa dawa, wafanyakazi wasio waadilifu ambao wanatumia nafasi zao vibaya wanashirikiana na baadhi ya wafanyabiashara na kuuza dawa, hili ni suala muhimu PST jadilianeni suala la maadili kwani hatua za kisheria dhidi yao zitachukuliwa"alisema

Awali Rais wa PST, Michael Kishiwa, aliiomba Serikali kuongeza udahili wa wanafunzi wa famasia wakiwemo mafamasia wasaidizi ili kutoa dawa sahihi kwa wagonjwa. Alisema hivi sasa idadi ya watanzania ni kubwa, lakini wataalamu wa dawa Wafamasia ni 1,200, hali inayochangia kuwepo kwa watoa huduma hiyo wasio na sifa. Alisema kutokana na kukosekana wanataaluma kumekuwepo na changamoto kubwa ya baadhi yao kukiuka maadili na wengine kufanya kazi ya utoaji dawa pasipokuwa na uelewa nayo, hali ambayo hatari kwa afya za binadamu.

Kishiwa alisema kazi kubwa ya chama chao kuhakikisha inasimamia ubora wa utoaji huduma ya dawa na kusimamia maadili, ili wananchi wapate dawa sahihi na kuzitumia ipasavyo. “Tunashirikiana na baraza la usajili la wafamasia katika kukemea vitendo hivyo vya ukiukwaji wa maadili na ndiyo maana tunaiomba serikali iongeze udahili na vyuo vinavyotoa taaluma hii"alisema

Naye Msajili wa Baraza la Wafamasia, Elizabeth Shekalage alisema kwa sasa wananchi wengi wamechukulia huduma ya dawa ni biashara na kuwa baraza limejipanga kupambana na watu wanaofanya huduma hiyo ni biashara huku wakikiuka maadili.

"Uchache wa wanataaluma unasababisha kika mtu aone hii ni biashara huria na yeyote anaweza kuifanya,kuna uhaba mkubwa wa fundi dawa sanifu,mafundi dawa wasaidizi,dawa ni sumu hivyo tunasimamia hili ili kuepusha madhara kwa watumiaji"alisema Elizabeth

Kongamano la Mwaka huu linaenda na kauli mbiu isemayo kuelezea ubora,usalama,ufanisi na upatikanaji wa huduma bora za kifamasia.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo akitoa hotuba katika ufunguzi wa kongamano la 49 la Chama cha Wafamasia Tanzania.

Rais wa Chama cha wafamasia Tanzania (PST) Ndg. Michael Kishiwa (aliyesimama)akitoa taarifa ya Chama kwa kifupi kwa Mgeni Rasmi Mhe. Mrisho Gambo katika Kongamano la 49 la wafamasia Tanzania linalofanyika Jijini Arusha.
Wanachama wa PST wakifuatilia ufunguzi wa Kongamano .
 

Wajumbe wa kongamano wakiendelea kufuatilia Hotuba ya Ufunguzi .
1. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo(Kushoto) akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na dawa Hiti Silo katika Kongamano la  wafamasia linalofanyika katika Jiji la Arusha. 
 


MKUU WA WILAYA YA UBUNGO, HAMFREY POLEPOLE MGENI RASMI MPAMBANO WA MABONDIA.

Na Mwandishi Wetu.
Mgeni rasmi katika
mpambano wa Mabondia  mbalimbali watakaozipiga siku ya jumapili ya Oktober 2 katika ukumbi wa White House Bar Kimara Korogwe 
atakuwa  Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole. 

 Mambondia hao watapima uzito pamoja na Afya zao kesho jumamosi katika ukumbi wa White haouse kwa ajili ya kuzipiga siku inayo fuata.

akizungumzia mpambano uho kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini ambaye ni mratibu wa mpambano uho Rajabu Mhamila 'Super D' amesema kuwa mabondia wote watapia uzito pamoja na Faya Zao siku ya jumamosi.

aliwataja baadhi ya mabondia watakaozipiga na kesho watapima uzito ni Said Chino atakaezitwanga na haidar Mchanjo uzito wa kg 57 raundi sita wakati Abdallah Ruwanje atavaana na Shedrack Ignas mpambano wa raundi sita la uzito wa kg 63wakati bondia mkongwe kabisa katika mchezo wa masumbwi nchini Mustafa Doto atazipiga na bondia chipkizi Manyi Issa katika uzito wa kg 61 raundi sita.

mipambano mingine itawakutanisha mabondia Mohamed Muhunzi atakaepambana na Kassim Ahmad na Hashimu Chisora atazipiga na Rojas Masam uzito wa kg 61 na Julias Jackson atapambana na Emilio Norfat mpambano wa raund 4 uzito wa kg 61 na Ellsame Mbwambo atazipiga na Emanuel Kisawani mpambano wa raundi 4 uzito wa kg 61.

siku hiyo pia kutakuwa na elimu ya ujasiliamali kwa vijana wa mchezo wa masumbwi pamoja na kupatiwa mafunzo mbalimbali ya kujikwamuwa na uchumi 

Katika Mchezo huo kutakua na Uzwaji wa DVD za mafunzo ya mchezo wa ngumi pamoja na kutambua sheria zake mbalimbali zitakazokua zikisambazwa na kocha 'Super D' kwa ajili ya kuwapa mabondia mbalimbali mbinu za mchezo na mashabiki kujua sheria za masumbwi. 

Ndani yake wakiwemo mabondia Floyd Mywether, Manny Paquaio, Amiri Khani, Mohamedi Ali, Mike Tayson David Haye na wengine ambapo kutakuwa na matukio ya mazoezi yao katika mataifa yao ikumbukwe kuwa ni mabingwa wa dunia. na kutakuwa na mapambano makubwa matano ya utangulizi.


KAMANDA MPINGA AONGOZA MSAFARA WA WAJUMBE NA WANAKAMATI WA USALAMA BARABARANI KUTEMBELEA MGODI WA GEITA(GGM).

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi Mohamed Mpinga wa tatu kutoka kulia na Wevyeviti, Wanakamati na Wajumbe wa Usalama Barabarani Nhini wakiangaliana moja shimo la Dhahabu  katika Mgodi  wa Geita (GGM) jana walipokwenda kuutembelea na kujifunza njia wanazotumia katika kuwakinga au kuwaepusha watumishi wa Mgodi huo na ajali zinazoweza kujitokeza maeneo yao ya kazi. 
 Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi Mohamed Mpinga, alievyaa Tishert  nyeupe  akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mgodi wa Geita Golg Mainng(GGM) jana baada ya ziara ya kuutembelea Mgodi huo katika Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yanayoendelea mkoani Geita.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi Mohamedi Mpinga, akimkabidhi zawadi mwanafunzi wa Geita shule ya msingi Suzi John baada ya kushinda katika shindano la uchoraji wa Picha za Usalama Barabarani jana katika  maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani yanayoendelea mkoani Geita.
  (Picha na Trafiki kuu).


BEI YA MADAFU LEO.TAARIFA YA KANUSHO KUHUSU TANGAZO LA AJIRA SERIKALININaibu Waziri wa Afya Dk. Kigwangalla afanya ziara Hospitali ya Mkoa wa Kigoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla amefanya ziara ya kikazi katika Hospitali ya Rufaa ya Maweni ya Mkoa wa Kigoma na kujionea mambo mbalimbali.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliweza kubaini mapungufu kadhaa ambapo amewataka uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha wanatatua matatizo hayo haraka. Miongoni mwa matatizo hayo ni pamoja na kutokuwa na mfumo maalum wa kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki ili kudhibiti mapato huku akiwataka ndani ya miezi mitatu wawe wameshakamilisha mfumo huo.

Mbali na hilo pia amewataka kuzingatia utunzaji wa vifaa vya Maabara ya Hospitali hiyo kwani licha ya kuwa na jingo zuri lakini bado hali ya utunzaji imekuwa ndogo na hata kusababisha vifaa vingine havifanyi kazi.

Kwa upande wa Chumba cha upasuaji (Theatre) amewaagiza kuhakikisha wanaondoa kasoro zote muhimu kwani Chumba hicho kimekosa sifa ya kuitwa Chumba cha Upasuaji cha Hospitali ya Mkoa wa Kigoma baada ya kushuhudia ufinyu wa jengo lenyewe, ukosefu wa vifaa na hali nzima ya sehemu ya utendeaji kazi.

Naibu Waziri wa Afya ametembelea Mkoa Kigoma katika ziara yake ya siku mbili, awali aliweza kutembelea Kituo cha Afya cha Uvinza kilichopo Wilaya ya Uvinza, pamoja na Hospitali ya Heri Mission iliyopo Wilayani Buhigwa Mkoani humo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla akipatiwa maelezo kutoka kwa msimamizi wa Maabara ya Hospitali ya Mkoa wa Kigoma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla akitoa maelezo ya maboresho.
Baadhi ya Madaktari na wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla (Hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao na kupata maoni yao juu ya utendaji kazi Hospitali hapo.