Na Lilian Lundo - MAELEZO - Dodoma
Uanzishwaji wa Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) kwa shule za Msingi za
Serikali Mkoani Dodoma umefanikiwa kutatua migogoro baina ya walimu na
wazazi iliyodumu kwa muda mrefu mkoani humo.
Hayo yamesemwa leo, Mjini Dodoma na Mratibu Elimu Kata wa Kigwe
Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma Elias Milaji katika Mkutano wa Waratibu
wa Elimu Kata wa Mkoa huo kuhusu Mafanikio ya uanzishwaji wa UWW
katika shule za Msingi za Serikali katika Mkoa huo.
"UWW umeweza kutatua migogoro mingi iliyoko katika kata ya Kigwe, moja
ya migogoro hiyo ni wazazi kugoma kushiriki mikutano ya shule kutokana
na walimu kukataa kuwafuta watoto wa kike shule ili wakaolewa,"
alifafanua Milaji.
Aliendelea kwa kusema kuwa, baada ya uanzishwaji wa UWW katika kata
hiyo migogoro imepungua kwa kiasi kikubwa na wazazi wamekuwa
wakishiriki katika kufuatilia maendeleo ya masomo pamoja na mahudhurio
ya watoto wao.
Kwa upande wake Mratibu Elimu Kata wa Chamwino, Chitema Simango
amesema kuwa UWW umewezesha kwa kiasi kubwa ushiriki wa wazazi katika
maendeleo ya shule ambapo kabla ya uanzishwaji wa Umoja huo walimu
walikuwa wakiachiwa ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi pamoja na
shule lakini kwa sasa wazazi na walimu wanashirikiana kwa pamoja
katika kufuatilia maendeleo ya wanafunzi na shule.
Aidha UWW umeleta uwazi katika mapato na matumizi ya shule ambayo
yanabandikwa katika mbao za matangazo za shule husika na wazazi
wanapewa nafasi ya kuhoji juu ya mapato na matumizi hayo.
UWW ni mpango ulionzishwa na Serikali kwa kushirikiana na Mpango wa
Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP-T) ukiwa na lengo la kuboresha
mahusiano bora kati ya walimu na wazazi. Umoja huo mpaka sasa
umeanzishwa katika mikoa ya Dodoma, Kigoma, Shinyanga, Simiyu, Tabora,
Mara na Lindi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...