Majadiliano kati ya Tanzania na timu ya wawakilishi wa kampuni ya Barrick Gold inayomiliki migodi ya madini hapa nchini yamekamilika na makubaliano kati ya pande hizo yametiwa saini leo tarehe 19 Oktoba, 2017 mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
Timu ya Barrick Gold Corporation ilikuwa imeongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo Prof. John Thornton wakati timu iliyowakilisha Serikali ya Tanzania imeongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi.
Miongozi mwa mambo waliyokubaliana ni kutekeleza mwelekeo mpya wa biashara ya madini ambapo kutakuwa na mgawanyo sawa wa faida (yaani Tanzania kupata asilimia 50 na Barrick Gold Corporation kupata asilimia 50 ya faida) na kuundwa kwa kampuni ya ubia wa usimamizi wa migodi ya madini iliyopo Tanzania ambayo itakuwa na makao makuu yake Mwanza na ofisi ndogo Dar es Salaam nchini Tanzania badala ya nchini Uingereza.
Mengine ni kufunga ofisi za uhasibu na fedha zilizopo Johannesburg Afrika Kusini na kuhamishia Tanzania na kutekeleza masharti yote ya mabadiliko ya sheria mpya ya madini na rasilimali za nchi ya mwaka 2017.
Aidha, Barrick Gold Corporation imekubali kuwepo kwa wawakilishi wa Serikali katika bodi za migodi yake yote hapa nchini, kazi mbalimbali za kwenye migodi kufanywa na kampuni za Kitanzania, Migodi kutoa ajira za kudumu kwa wachimbaji, wachimbaji hao kuishi majumbani kwao badala ya kuishi kwenye makambi ya migodi na mashauri yote ya kesi mbalimbali kufanywa hapa nchini.
Kampuni ya Barrick Gold pia imekubali kutoa Dola za Kimarekani Milioni 300 sawa na takribani Shilingi Bilioni 700 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kupitia biashara ya kampuni hiyo.
Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo Prof. Thornton amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa msimamo wake unaojenga misingi ya biashara ya kuaminiana na uwazi, ambayo ni muhimu na ya namna yake kwa biashara katika karne hii ya 21.
Prof. Thornton amesema Barrick Gold Corporation watazingatia makubaliano haya na wanaamini kuwa yamefungua ukurasa muhimu utakaowezesha kufanya biashara kisasa.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amezipongeza timu zote mbili yaani Tanzania na Barrick Gold Corporation kwa kazi kubwa ziliyofanya kufikia makubaliano hayo na kwa kipekee amempongeza Prof. Thornton kwa nia yake thabiti ya kukubali kufanyika kwa mazungumzo na kukubali mambo yaliyofikiwa.
Mhe. Rais Magufuli amesema makubaliano hayo yataisaidia nchi kuzalishaji ajira zaidi, kupata manufaa mbalimbali yanayostahili ikiwemo fedha za kugharamia huduma za kijamii kwa wananchi na yanajenga msingi imara ambao utaiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zake za madini.
Mhe. Dkt. Magufuli amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi kuunda timu zitakazoshughulikia biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi pamoja na migodi mingine ya dhahabu haraka iwezekanavyo ili nchi iweze kunufaika ipasavyo.
“Nataka machimbo yote ya dhahabu mchakato kama huu ufanyike, pia nakuagiza Prof. Kabudi biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi nako ni lazima kufuate utaratibu huu, asiyetaka aondoke” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Pia Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi badala ya baadhi yao kuzibeza kwa kuwa zina manufaa kwa taifa na wananchi wake. 
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Oktoba, 2017 
 Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation Profesa John L. Thornton akiwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Jumanne jioni tayari kushiriki katika mazungumzo ya mwisho na hatimaye makubaliano baina ya Kamati ya serikali na timu ya wataalamu wa kampuni hiyo kuhusiana na makinikia pamoja na biashara ya madini kwa ujumla. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimlaki  Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corp.Profesa John L. Thornton alipokutana nae wakati wa kupokea ripoti ya makubaliano baina ya Kamati ya Serikali na  timu ya wataalamu wa Barrick Gold kuhusu bishara ya madini Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 19, 2017
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea  na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corp.Profesa John L. Thornton alipokutana nae wakati wa kupokea ripoti ya makubaliano baina ya Kamati ya Serikali na  timu ya wataalamu wa Barrick Gold kuhusu bishara ya madini Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 19, 2017
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corp. Profesa John L. Thornton akiwa na Afisa Uendeshaji wa Barrick Gold  Richardc William huku Waziri wa Sheria na Katiba Profesa Palamagamba Kabudi na Florens Luoga nao pia wakiweka saini ripoti ya makubaliano baina ya Kamati ya Serikali na  timu ya wataalamu wa Barrick Gold kuhusu bishara ya madini Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 19, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corp. Profesa John L. Thornton akiwa na Afisa Uendeshaji wa Barrick Gold  Richardc William huku Waziri wa Sheria na Katiba Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Florens Luoga nao pia wakiweka saini ripoti ya makubaliano baina ya Kamati ya Serikali na  timu ya wataalamu wa Barrick Gold kuhusu bishara ya madini Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 19, 2017

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...